Mwili wa , Joshua Mollel (21), kijana Mtanzania aliyeuawa nchini Israel katika shambulio la Hamas la Oktoba 7,2023 unatarajiwa kuwasili leo Novemba 19, 2025, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), na kukabidhiwa kwa familia na mamlaka za Serikali kwa taratibu za mazishi.
Taarifa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Israel inasema ibada fupi ya kumuaga Mollel ilifanyika jana Jumanne, katika mnara wa kumbukumbu jijini Tel Aviv, ikiangazia mchango wake na namna maisha yake yalivyokatishwa ghafla kutokana na ghasia hizo.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Israel, Alex Kallua na maofisa wa ubalozi.
Mollel alikuwa nchini humo kwa ajili ya mafunzo ya kilimo katika eneo la Kusini mwa Israel wakati shambulio hilo lilipotokea mnamo Oktoba 7, 2023. Alipoteza maisha katika eneo la Kibbutz Nahal Oz, na mwili wake kuchukuliwa na washambuliaji wakati wa mashambulizi hayo.
Kwa mujibu wa taarifa za Israel, mwili wa Mollel ni miongoni mwa miili ya mateka watatu wa kigeni akiwemo mmoja kutoka Thailand na mwingine kutoka Nepal iliyorejeshwa kufuatia makabidhiano ya miili yaliyofanyika hivi karibuni. Taifa hilo pia limekabidhi miili ya Wapalestina 285 badala ya miili ya mateka 19 wa Israel iliyorejeshwa na Hamas.
Familia, marafiki na Watanzania kwa ujumla wanatazamiwa kuungana leo kutoa heshima za mwisho kwa kijana huyo aliyekuwa akitekeleza ndoto zake za kujifunza kilimo nje ya nchi, kabla ya kuuawa.