Mkazi wa kijiji cha Isaka kata ya Nkunga Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya Derick Mwangama (23) ameripotiwa kumuua mtoto wake Deniva Derick mwenye umri wa Miaka Miwili, kwa kumnyonga hadi kufa kwa kutumia kamba ya manila na yeye kujinyonga na kupoteza maisha.
Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga leo Novemba 21, 2025 na kusema tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Isaka, Novemba 18, 2025.
Kamanda Kuzaga amesema awali kabla ya tukio hilo baba mzazi wa mtoto huyo ambao wote ni marehemu, alikwenda nyumbani kwa mzazi kwenzie Violeth Edward (19) na kumchukua kwa nguvu mtoto huyo huku akiwa na jazba.
Amesema baada ya kuondoka naye, baadaye mwili wa mtoto ulikutwa ukiwa umenyongwa na kisha kutekelezwa kando ya Mto Kiwira.
Aidha Kamanda Kuzaga amesema baba wa mtoto huyo ambaye ni marehemu baada ya kufanya mauaji hayo ya mwanaye, alijinyonga kwa kutumia kamba ya manila kwenye mti wa parachichi kando ya mwili wa mtoto wake.
“Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio hilo ni kuibuka kwa mgogoro baina wenza hao ambao walikuwa wametengana,” amesema.