Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemwagiza Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, kulifungulia Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, baada ya kukumbwa na changamoto za kiuendeshaji zilizosababisha kufutiwa usajili wake.
Akizungumza leo, Novemba 24, 2025, katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Jimbo la Kibamba, jijini Dar es Salaam, Dkt. Mwigulu amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa baadhi ya taasisi za kidini zilizopitia misukosuko, na kuagiza zifanyiwe tathmini upya.
“Namwagiza Waziri wa Mambo ya Ndani kufuatilia utaratibu mzuri. Ziandikwe upya taasisi za kidini, zisisitizwe miiko na masharti yao. Zile zilizokuwa na changamoto zipewe miezi sita ya uangalizi. Natambua kuwepo kwa taasisi ya Ufufuo na Uzima; ifunguliwe na wapewe masharti ya uangalizi ndani ya miezi sita,” amesema Waziri Mkuu.
Ameongeza kuwa ni muhimu taasisi zote za kidini kukumbushwa kuzingatia miiko ya utendaji, masharti ya usajili na sheria za nchi.
Dkt. Mwigulu amesema makosa ya taasisi moja hayapaswi kuwa sababu ya kuzifungia taasisi nyingine, akibainisha kuwa ibada ni uhusiano kati ya mtu na Mungu wake, hivyo vitendo vya baadhi ya viongozi havipaswi kuwanyima waumini haki yao ya kuabudu.