Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amelielekeza Jeshi la Polisi kusitisha kumtafuta Askofu. Josephat Gwajima kama lilivyotangaza awali, ili apate kuendelea na shughuli zake na kutoa fursa ya kujenga umoja wa kitaifa.
Akizungumza leo (Jumapili, Novemba 30, 2025) katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Magufuli–Leganga, Usa River wilayani Arumeru, Mwigulu amesema kuwa baada ya Kanisa la Ufufuo na Uzima kupewa msamaha, ni muhimu kiongozi wake akatokeza hadharani kuendelea na majukumu yake.
“Mwacheni ajitokeze. Waumini wanamhitaji. Tujenge umoja wa kitaifa, tushikamane kurudisha amani. Tumekutana na TEC, viongozi wa dini na wa mila; twendeni sote kwenye wito huu wa Mheshimiwa Rais,” amesema.
Amesema Rais Samia ametuma salamu kwa wananchi wa Arumeru na kutambua changamoto walizopitia, ikiwemo vurugu zilizotokea hivi karibuni. “Anatambua yanayotokea, anatambua kazi mnayofanya kujenga Taifa,” amesema Mwigulu.
Kabla ya mkutano huo, Waziri Mkuu alikagua athari za vurugu za Oktoba 29, 2025 ikiwemo kuchomwa moto kwa kituo cha polisi cha Kikatiti, Mahakama ya Mwanzo ya Maji ya Chai na kituo cha mafuta cha Total Energies, pamoja na uporaji na uharibifu wa mali.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwigulu, maendeleo katika maeneo kama maji na barabara hayataweza kutekelezwa endapo nchi itaendelea kuwa kwenye misukosuko. “Tukichagua vurugu tunachagua kufukuza maendeleo na kuongeza umaskini,” ameonya.
Ameeleza kuwa uchochezi mwingi unatoka kwa watu waliopo nje ya nchi, akidai kuwa baadhi ya vijana wanaoishi nje wamepokea dola milioni mbili (sawa na shilingi bilioni 4.5) kwa ajili ya kuchochea vurugu. “Wanalipwa ili kutuvuruga. Wana ajenda gani na nchi yetu? Tunajua watazirudishaje hizo fedha?” amehoji.
Amesema kuwa chanzo cha juhudi za kuwavuruga Watanzania ni rasilimali zinazogunduliwa ikiwemo uranium, ambapo Tanzania sasa ina tani 890,000 za ujazo na kuwa nchi ya tisa duniani na ya kwanza Afrika. “Wanalenga tupigane ili wachukue rasilimali. Tumeshuhudia hili likiharibu mataifa mengi ya Afrika,” amesema.