WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde ameagiza Ofisi ya Madini mkoa Kimadini Mbogwe kufanya uchunguzi wa leseni kubwa za utafiti (PL) 191 ambazo hazijaendelezwa kwa muda mrefu.
Mavunde ametoa maagizo hayo akiwa wilayani Nyang’hwale mkoani Geita wakati wa hafla ya ugawaji wa leseni kwa vikundi vya wachimbaji wadogo iliyofanyika katika kijiji cha Nyijundu.
Amesema kabla ya uchunguzi taarifa ya awali ya leseni hizo inapaswa kuwasilishwa ofisini kwake Jumatano ya Desemba 03, 2025 ikiainisha wamiliki na mwenendo wa uendelezaji wa leseni hizo.
“Hizo leseni 191 za Geita zinafanya nini hapa, mpaka leo mkoa wa kimadini wa Mbogwe hauna mgodi mkubwa, huo utafiti wao ni wa nini, hii habari ya kushikilia maeneo ni lazima ikome”.