Makao makuu mapya ya Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), yamezinduliwa rasmi jijini Kisumu, Kenya, hatua muhimu inayolenga kuimarisha utafiti, uratibu na ubunifu kuhusu changamoto za mazingira, uchumi na kijamii katika Bonde la Ziwa Victoria.
Jengo hilo jipya, lililojengwa kandokando ya Ziwa Victoria, limeelezwa kuwa nguzo ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kulinda rasilimali za umajumui huu mkubwa barani Afrika.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Rais William Ruto, Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Maeneo Kame na Maendeleo ya Kikanda, Beatrice Askul, amesema uzinduzi huo unaonyesha dhamira ya pamoja ya nchi wanachama kulinda ikolojia ya ziwa hilo kupitia sera shirikishi, utafiti wa kisayansi, na juhudi za pamoja kupambana na uchafuzi wa mazingira.
Amebainisha kuwa makao hayo mapya yatatumika kama kitovu cha umahiri katika masuala ya utafiti, ubunifu na uongozi wa sera zitakazosaidia kusimamia rasilimali za bonde hilo kwa njia endelevu, ikiwemo usimamizi wa uvuvi mpakani na kuimarisha mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Askul ameongeza kuwa Serikali ya Kenya inaendelea kuimarisha miundombinu katika eneo hilo kupitia upanuzi wa reli, ujenzi wa barabara za mpakani na uundaji wa vituo vya uratibu wa usalama majini ili kuimarisha shughuli za kiuchumi na usafirishaji.
Amesisitiza kuwa Kenya imejipanga kushirikiana na nchi wanachama wa EAC ili kujenga ukanda imara, wenye umoja na ustawi, ikiwemo kuendeleza miradi ya miundombinu kama upanuzi wa reli ya kisasa (SGR).
Kwa upande wao, Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva, Naibu Gavana wa Kisumu, Dk. Mathews Owili, na Katibu Mtendaji wa LVBC, Dk. Masinde Bwire kwa nyakati tofauti wametilia mkazo umuhimu wa kuhakikisha ofisi hiyo mpya inakuwa kitovu cha suluhisho la changamoto za mazingira na kijamii zinazolikabili eneo la Ziwa Victoria.
Ujenzi wa jengo hilo la kisasa ulianza mwaka 2020 na kukamilika kwa gharama ya dola milioni 3.54, zikiwa ni michango sawa ya nchi wanachama wa EAC, na sasa limekuwa jengo la kwanza la EAC kujengwa nchini Kenya.