Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema kuwa serikali tayari imeanza kutekeleza ajenda ya kuwa na viwanda vya dawa na vifaa tiba ili kuhakikisha bidhaa hizo zinazalishwa kwa wingi na viwanda vya ndani, jambo ambalo litachochea maendeleo ya nchi.
Mchengerwa ametaja hatua ambazo tayari serikali imezitekeleza, akieleza mojawapo ni ujenzi wa kituo cha uzalishaji dawa cha Mloganzila na Kibaha mkoani Pwani.
Ameeleza hayo leo Januari 19, 2026 katika mkutano wa wawekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba wa ndani na nje ya nchi, uliofanyika katika Hoteli ya Kilimanjaro Hyatt Regency, Dar es Salaam.
Waziri Mchengerwa amesema kuwa vituo hivyo vinajumuisha na kuwaleta pamoja wazalishaji wa bidhaa za dawa na vifaa tiba, wasimamizi wa sekta hiyo, watafiti pamoja na miundombinu ya usafirishaji.
Aidha, amesema uwepo wa vituo hivyo umeongeza viwango vya ubora pamoja na kupunguza gharama za uzalishaji wa dawa na vifaa tiba.
Aidha, ametoa wito kwa wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani kufanya uwekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba nchini, huku akiwahakikishia kuwa serikali ya Tanzania imeboresha mazingira ya uwekezaji na kwamba hawatakutana na vikwazo wala usumbufu wowote.
Tanzania imewekeza dola milioni 10 za Marekani katika kununua miundombinu ya maabara za kuzalisha dawa katika vituo hivyo, huku akisisitiza kuwa miundombinu hiyo itasaidia kupunguza muda wa kutafuta masoko pamoja na kusaidia bidhaa hizo kukidhi matakwa ya sheria na miongozo ya kimataifa ikiwemo ile inayotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO).