Msanii Harold Simmons II, anayefahamika kwa jina la kisanii Fyütch, ameandika historia baada ya kuteuliwa kuwania tuzo ya Grammy kwenye kipengele cha Best Children’s Music Album pamoja na binti yake wa miaka 8, Aura V.
Fyütch alianza safari yake ya muziki tangu akiwa shule ya sekondari, akianzisha bendi ya jazz na hip-hop kabla ya kuendelea peke yake. Baadaye, alipokuwa mwalimu, alianza kutengeneza muziki wa kielimu kwa watoto, hatua iliyomfungulia njia mpya ya ubunifu na mafanikio.
Aura alianza kuambatana na baba yake kwenye matamsha alipokuwa hajaanza shule. Mwanzoni alikuwa na wasiwasi kupanda jukwaani, hasa mbele ya watoto wanaomzidi umri, lakini kwa muda ameongezeka kujiamini na sasa anaweza kutumbuiza mbele ya mashabiki wa rika zote.
Katika miaka ya hivi karibuni, duo hii ya baba na binti imepanda majukwaa makubwa na maarufu duniani kama Lincoln Center na Carnegie Hall, wakionyesha muziki wao wa asili unaolenga familia. Nominisheni yao ya Grammy imewafanya kuwa miongoni mwa familia chache sana zilizofanikisha ushindi mkubwa kwa pamoja kwenye kiwanda cha muziki.