
Mtu mmoja amefariki dunia, baada ya basi la abiria kugongana uso kwa uso na lori la mizigo katika Kitongoji cha Kitongo kata ya Butengorumasa, Wilaya ya Chato mkoani Geita
Ajali hiyo imehusisha basi la Kampuni ya Mallesa lenye namba za usajili T 708 DPS lililokuwa likitokea jijini Dar es Salaam kwenda mkoani Geita kugongana na lori aina ya Mitsubishi Canter T 573 DZW lililokuwa likisafiri kutoka mkoani Mwanza kuelekea wilayani Kibondo mkoani Kigoma.
Kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Adamu Maro amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa imetokea Oktoba 07, 2025 majira ya saa 8 usiku ambapo amemtaja aliyefariki kuwa ni dereva wa gari la mizigo Said Ramadhan (23) na mwili wake umehifadhiwa katika kituo cha afya Katoro kwa taratibu za uchunguzi kabla ya hatua za mazishi.
Aidha Kamanda Maro amesema kuwa abiria wawili ambao ni Anastazia Yohana (25) na Ismail Omari (34) wote wakazi wa Dar es Salaam wamepata majeraha na wanaendelea kupata matibabu katika kituo cha Afya Katoro na abiria wengine wapo salama.
“Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa Mitsubishi Canter, alihama upande wake na kwenda upande wa kulia pasipo kuchukua tahadhari au kuzingatia watumiaji wengine wa barabara kisha kuligonga basi”, amesema kamanda Maro