Jeshi la Polisi nchini limethibitisha kumshikilia Ambrose Dede, kwa tuhuma za kupanga na kuhamasisha uhalifu kupitia kundi la WhatsApp lijulikanalo kama “Sauti ya Watanzania.”
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 13, 2025 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, Dede amekamatwa eneo la njia panda ya Makiungu, Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.
“Kulingana na ushahidi uliokusanywa kabla na baada ya kukamatwa kwake, inaonyesha kuwa katika kundi hilo la WhatsApp, mtuhumiwa ni miongoni mwa wasimamizi wa kundi hilo (Group Admins),
Amekuwa akishirikiana na watu waliopo ndani na nje ya nchi kupanga na kuhamasisha uhalifu kwa mwavuli wa maandamano ya amani,” amesema Misime.
Ameongeza kuwa uchunguzi unaendelea kukamilishwa, ikiwemo kuwatafuta wengine wanaoshirikiana na mtuhumiwa kupitia namba za simu ambazo hazijatajwa kwa sababu za kiuchunguzi.
“Baada ya uchunguzi kukamilika, hatua nyingine za kisheria zitafuata,” taarifa hiyo ya polisi imeeleza.
Aidha, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kujiepusha na makundi ya mawasiliano mtandaoni yanayoendeshwa na watu wanaopanga au kuhamasisha uvunjifu wa amani nchini.
“Tunatoa wito kwa wananchi wote kuepuka kujihusisha na makundi ya aina hiyo.
Uhalifu hauwezi kufichwa chini ya mwavuli wa maandamano ya amani.
Hatutasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote atakayebainika,” ameonya Misime.
Misime ameongeza kuwa watu wanaopanga na kuhamasisha vurugu hizo hawapati madhara yoyote, bali ni Watanzania wa kawaida wanaoumizwa na matokeo ya vitendo hivyo.
“Ni vizuri kila mmoja wetu kutambua kuwa watu wa aina hiyo wanaendelea kunufaika na fedha wanazolipwa kupitia makundi hayo ya mtandaoni, huku wananchi wakiwa ndio waathirika wakuu,” alisema.