Binti anayejulikana kwa jina la Anu Adeleke, anayejitambulisha kama mtoto wa mwanamuziki wa Nigeria David Adeleke (Davido), ameibua mjadala mkubwa baada ya kuandika barua ya wazi akiomba kufanyiwa kipimo cha DNA na msanii huyo ili kuthibitisha utambulisho wake.
Kwenye ujumbe wake, Anu amesema amekuwa akikumbana na changamoto kubwa tangu akiwa na umri wa miaka sita, akidai kubaguliwa na kuonewa shuleni baada ya kudai kuwa baba yake ni Davido. Hali hiyo, kwa mujibu wake, Ilimsababishia maumivu ya kisaikolojia hadi kulazimika kupata msaada wa kitaalamu wa afya ya akili.
Licha ya changamoto hizo, Anu anasema hakukata tamaa, bali alijituma masomoni na kufanikiwa kuwa miongoni mwa wanafunzi bora, akiwahi hata kuchaguliwa kuwa kiranja wa darasa. Ameeleza kuwa kwa sasa akiwa shule ya sekondari, ameamua kujikita zaidi kwenye masomo na kujenga maisha yake bila kuzungumzia historia ya familia yake.
Hata hivyo, akielekea katika hatua ya utu uzima, Anu amesema anaona ni haki yake kuomba kipimo cha DNA ili kupata ukweli na amani ya moyo. Amesisitiza kuwa ombi hilo ni la heshima na ni kati yake na Davido pekee.
Ujumbe huo, uliowekwa wazi kwa umma na pia kutumwa moja kwa moja kwa Davido kupitia DM, umeibua hisia mseto kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, huku wengi wakimpongeza kwa ujasiri wake na wengine wakisubiri majibu kutoka kwa familia ya Adeleke.