
Mwili wa Askofu Novatus Rugambwa umezikwa leo, Septemba 29, 2025, katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma, Bukoba mkoani Kagera.
Hayati Rugambwa amezikwa jirani na Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, Kardinali wa kwanza barani Afrika na aliyemrithisha jina lake pamoja na marehemu Askofu Nestor Timanywa, aliyemlea na kumpa daraja la upadri.
Misa Takatifu ya mazishi iliyohudhuriwa na maaskofu mbalimbali, viongozi wa dini na viongozi wa Serikali, imeongozwa na Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora.
Akizungumza wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya kumuombea na kumuaga askofu huyo aliyekuwa Balozi wa Papa, Kardinali Rugambwa amesema kifo chake kimewasikitisha wengi, hasa baada ya afya yake kudhoofika kutokana na shambulio la kiharusi.
Aidha Kardinali Rugambwa amewataka Waumini wa kanisa katoliki kuendelea kumuenzi kwa vitendo hayati balozi askofu mkuu Novatus Rugambwa aliyesifika kwa utu, upendo na ucha Mungu.
Aidha, ameeleza kuwa mchango wake haukuishia Bukoba pekee, bali ulienea katika majimbo na jamii mbalimbali nchini Tanzania.
Amesema kuwa alimfahamu vizuri askofu Rugambwa wakati wa utume wake ambapo alimheshimu kila mmoja bila kubeba wadhifa wake na pia alijitoa kuwasaidia wasiojiweza na kwamba ni vyema kila muumini akamuenzi ili kuendelea kustawisha mbegu yake hiyo.
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa na Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba, Jovitus Mwijage, wamemshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya askofu huyo wakielezea yalijaa matendo ya upendo hasa kwa watoto maskini.
Naye Balozi wa Papa nchini Tanzania Angelo Accattino akiwamikisha Papa LEO wa 14 amesema kuwa wanajivunia utume uliotukuka kutoka kwa askofu mkuu Rugambwa na kwamba kanisa katolikili Duniani linaungana na waumini wa jimbo Katoliki la Bukoba kusheherekea matunda yake na kwamba ataenziwa kwa mema aliyoacha.
Akisoma wasifu wa marehemu, Katibu wa Jimbo Katoliki Bukoba, Padri Prudence Mujwahuzi amesema alizaliwa Oktoba 8, 1957, kijiji cha Misengi, Parokia ya Maruku, Wilaya ya Bukoba.
Alibatizwa Novemba 1957, akapata komunio ya kwanza Novemba 22, 1964 na Kipaimara Julai 22, 1965.
Elimu ya msingi aliipata katika Shule ya Nyakatare (1963–1967) na Seminari Ndogo ya Mtakatifu Don Bosco Rutabo (1968–1971).
Kati ya mwaka 1972 hadi 1975, alisoma kidato cha kwanza hadi cha nne Seminari ya Rubya, kisha kidato cha tano na sita Seminari ya Mtakatifu Karoli Boromeo, Itaga, Jimbo Kuu Katoliki Tabora.
“Mwaka 1977 hadi 1978 alihudumu katika Jeshi la Kujenga Taifa, Bulombola Kigoma, kabla ya kujiunga na Seminari Kuu ya Mtakatifu Antoni, Ntungamo (1978–1980). Baadaye alisomea thiolojia Roma katika Chuo cha Kipapa Urbaniana.
Amesema mwaka 1984 hadi 1985 alifanya mwaka wa kichungaji katika Seminari ya Mtakatifu Maria Rubya na Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji, Ishamba.
Alipata daraja la Ushemasi Januari 6, 1986 na daraja la Upadri Julai 6, 1986 kwa mikono ya marehemu Askofu Nestor Timanywa.
Ugonjwa na mauti yake
Kwa mujibu wa Padri Mujwahuzi, Askofu Rugambwa alianza kuugua Oktoba 29, 2023, baada ya kupata kiharusi kikali akiwa kwenye utume wake wa kidiplomasia.
Alilazwa katika hospitali mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Wellington, Hospitali ya Kenepool na baadaye Hospitali ya Gemelli jijini Roma, Italia.