Msanii mkongwe wa muziki nchini, Ambwene Yesaya (AY), amewataka wasanii wa Tanzania kujenga utamaduni wa kusafiri nje ya mipaka ya nchi ili kupanua wigo wa fursa, kupata uzoefu mpya na kukuza thamani ya kazi zao katika soko la kimataifa.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa safari hizo, AY amesema kusafiri kunamsaidia msanii kupata exposure, kujifunza mbinu mbalimbali ndani ya tasnia ya muziki pamoja na kufungua milango ya ushirikiano na wasanii wa mataifa mengine.
Ametoa mfano wa wasanii wa kimataifa akiwemo Victoria Kimani, Yemi Alade na Patoranking, akieleza kuwa waliwahi kuja nchini Tanzania kufanya maonesho ya Fiesta kwa gharama zao bila malipo. Hata hivyo, baada ya kujijengea umaarufu kwa mashabiki wa Tanzania, walirejea tena na kuhitaji malipo makubwa zaidi.
Kupitia mfano huo, AY amesisitiza kuwa thamani ya msanii inaweza kuongezeka kulingana na juhudi anazoweka katika kujitangaza kimataifa, kwani mara nyingi hutambuliwa zaidi nje kabla ya kuthaminiwa ndani ya nchi.
Aidha, msanii huyo amesema ataendelea kuwa mfano kwa vitendo kwa kuendelea kusafiri katika nchi mbalimbali, ikiwemo Zambia, kwa lengo la kujifunza zaidi na kupanua mtandao wake ndani ya tasnia ya muziki.
