
Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Hesron Polepole, ametangaza rasmi kujiuzulu nafasi yake akitaja kukosekana kwa uelekeo sahihi katika uongozi wa kitaifa, kufifia kwa maadili na dhamira ya kuhudumia wananchi.
Kupitia barua aliyomwandikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Leo Polepole amesema amefikia hatua hiyo baada ya kujitafakari kwa kina na kwamba utulivu wa dhamira, baada ya kushuhudia kwa muda mrefu hali ya mambo ambayo kwa maoni yake “inateteresha maslahi mapana ya Taifa.
Polepole amehudumu kama Balozi wa Tanzania nchini Malawi kuanzia Machi 2022 hadi Aprili 2023, na baadaye kuhamishiwa Cuba, akihudumu pia kwa nchi rafiki za Karibe, Amerika ya Kati na baadhi ya mataifa ya Amerika ya Kusini hadi alipojiuzulu leo.
Katika barua yake amesema ameshuhudia mchakato wa kutafuta wagombea ndani ya chama cha mapinduzi umeonekana kuenda kinyume na tamaduni za uchaguzi ndani ya chama na dhamira ya kuwatumikia wananchi kuyumba.
Aidha Polepole amemshukuru Rais Samia kwa kumpa fursa ya kuitumikia nchi kama balozi kwa mataifa mbalimbali na kwamba ataendelea kuwa mwanachama wa chama cha Mapinduzi CCM.