
Zaidi ya shilingi bilioni 39 zimetengwa na Serikali kwa ajili ya kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria na kuwanufaisha wakazi wa Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera ili kuwaondolea changamoto ya kutumia maji visima na mito ambayo haina uhakika.
Rais na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema hayo leo hii October 15, 2025 akiwa katika Uwanja wa Zimbihile Wilayani Muleba kwenye kampeni za kuomba kura.
Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa anatambua katika Wilaya hiyo kuna changamoto kubwa ya uhaba wa maji hali ambayo imekuwa ikiwalazimu wananchi kutumia vyanzo ambavyo vinakauka muda wa kiangazi.
Awali Mgombea Ubunge Jimbo la Muleba Kusini Dkt. Oscar Kikoyo ameomba kutatua changamoto ya umeme kwenye visiwa ambavyo vipo ziwa Victoria kwani wanatumia umeme ambao hauna uhakika.
Naye Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amemshukuru Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uamuzi wake wa kuendeleza ujenzi wa Bonde la Mto Ngono, mradi ambao ulikuwa umesalia katika makabrasha ya Mpango wa Maendeleo wa Kwanza wa Nchi. Amesema serikali imeamua kutumia shilingi bilioni 500 kukamilisha ujenzi huo muhimu kwa wananchi wa Kagera.
Amezungumza hayo katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika mji wa Kayanga wilaya ya Karagwe mkoani Kagera , ambapo alieleza kuwa Bonde hilo ni uhai wa wananchi wa wilaya zaidi ya nne mkoani humo.
Alifafanua kuwa wazo la Bonde la Mto Ngono lilibuniwa na Askofu Kibira pamoja na Shehe Katura, likihusisha maeneo kuanzia Bukoba Vijijini hadi Misenyi. Hata hivyo, kwa muda mrefu lilikuwa limebaki katika makabrasha ya mipango ya maendeleo ya awali.
Aidha, alisema wananchi wa Kagera, hasa wa Karagwe na Kyerwa, wanahitaji vituo vya biashara, na kupitia mradi wa ACDP 1 serikali imeweka masoko matatu katika mkoa wa Kagera — moja likiwa Ngara na mawili Kyerwa. Aliongeza kuwa wakandarasi wapo kazini kwa ajili ya kujenga masoko hayo ambayo yalikwama kwa zaidi ya miaka 15.