
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekanusha taarifa zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa taasisi hiyo imechapisha fedha na kuzisambaza kwa ajili ya kugharamia uchaguzi mkuu, ikieleza kuwa madai hayo hayana ukweli wowote, ni upotoshaji unaolenga kupotosha umma.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025, na kusainiwa na Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba, BoT imesema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakihamasishwa kuondoa fedha zao kwenye benki za biashara kwa madai kuwa zinaishiwa fedha kutokana na uchaguzi.
Hata hivyo, BoT imesisitiza kuwa taarifa hizo pia ni za uongo na zinapaswa kupuuzwa na umma.
“Ninapenda kuwafahamisha wananchi wote kuwa taarifa hizo si za kweli, zinapaswa kupuuzwa na kukemewa wote wanaozisambaza,” imesema taarifa hiyo.
Aidha, BoT imefafanua kuwa, kama ilivyo katika nchi nyingine duniani, kuchapisha fedha hufanywa kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu, Sura ya 197, Benki Kuu ina jukumu la kuzungusha kiasi cha fedha kinachohitajika katika shughuli za kiuchumi pamoja na mahitaji ya kubadilisha fedha zilizochakaa.
Aidha, imebainisha kuwa fedha hizo huingizwa kwenye mzunguko kupitia benki za biashara na si vinginevyo, na kwamba mchakato huo hufanyika kwa kufuata taratibu rasmi ili kuhakikisha sera za fedha na utulivu wa bei unadhibitiwa ipasavyo.