Takribani Watu 70 hawajulikani walipo baada ya boti kuzama mtoni Mkoani Kasai katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Taarifa iliyotolewa jana Novemba 19, 2025 na Redio ya Umoja wa Mataifa, boti hiyo ilikuwa ikielekea mji mkuu, Kinshasa ikitokea bandari ya Bena Dibele umbali wa zaidi ya kilomita 800 wakati ilipozama siku ya Jumatatu katika Mto Sankuru
Boti hiyo ilikuwa imebeba karibu watu 120 na Watu wapatao 50 wameokolewa hadi sasa, na juhudi za kutafuta wengine waliopotea zinaendelea kwamjibu wa ripoti hiyo ikimnukuu msimamizi wa eneo hilo Francois Ahoka.
Ahoka ameashiria ugumu zinaokabiriana nao timu za uokoaji na kutoa wito kwa familia kuwasiliana na mamlaka za mitaa kuwatambua manusura na miili iliyopatikana.
Usafiri wa majini ni jambo la kawaida nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na tatizo la ubovu wa barabara nyingi ambazo hazipitiki.
Ajali za majini zinazosababisha maafa ya roho za watu zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara katika nchi hiyo.
Katikati mwa mwezi Septemba mwaka huu, watu takribani 193 walifariki dunia katika matukio mawili ya kuzama boti yaliyotokea tarehe 10 na 11 maeneo ya kaskazini-magharibi mwa jimbo la Equateure