
Rapa Cardi B anakabiliwa na kesi ya hakimiliki baada ya kuposti picha yake mwenyewe kwenye mitandao ya kijamii.
Oktoba 1 mpiga picha Jawad Elatab alimfungulia kesi katika Mahakama ya Wilaya ya New Jersey, akidai kuwa Cardi alivunja haki zake za ubunifu.
Kwa mujibu wa hati za mahakama, Elatab ndiye aliyepiga picha ya Cardi B akiwa amevalia suti ya mpira ya rangi ya zambarau kwenye sherehe ya Netflix, na alisajili picha hiyo rasmi katika Ofisi ya Hakimiliki ya Marekani mwaka 2019.
Hata hivyo, Aprili 2021, Cardi aliposti picha hiyo kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) bila idhini ya mpiga picha, jambo ambalo Elatab anadai ni uvunjaji wa haki miliki.
Kesi hiyo sasa ipo mikononi mwa mahakama huku mashabiki wengi wakijadili iwapo mtu anaweza kweli kushitakiwa kwa kuposti picha yake mwenyewe.