Marehemu Chadwick Boseman, anayekumbukwa duniani kwa uhusika wake kama T’Challa (Black Panther) na kwa kuigiza historia ya mashujaa wakubwa kama Jackie Robinson, James Brown na Thurgood Marshall, amepewa heshima ya kipekee baada ya kutunukiwa nyota ya Hollywood Walk of Fame miaka kadhaa baada ya kifo chake.
Katika hafla hiyo maalum iliyofanyika Hollywood Boulevard, mjane wake Simone Ledward-Boseman alipokea nyota hiyo kwa niaba yake, huku akitoa maneno ya kugusa akisema Chadwick alikuwa mtu mwenye moyo mpana na aliyeishi kwa ajili ya watu.
Mkurugenzi Ryan Coogler, aliyefanya naye kazi kwenye Black Panther, alisifu nidhamu ya Boseman, akisema alibadilisha namna dunia inavyoangalia mashujaa wa Kiafrika na kuwainua vijana wengi barani Afrika na diaspora.
Mwimbaji na mwigizaji Viola Davis naye alitoa heshima zake akisema, “Nyota hii inang’aa kidogo kuliko Chadwick anavyong’ara mbinguni leo.”
Chadwick Boseman alifariki mwaka 2020 kutokana na saratani ya utumbo mpana, lakini kazi zake, roho yake, na athari yake kwenye utamaduni zimeendelea kuishi na kuhamasisha vizazi vipya.
Kupata nyota kwenye Walk of Fame ni uthibitisho mwingine wa urithi wake usiokufa katika tasnia ya filamu duniani.