
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaahidi wakazi wa Mwanza kuwa endapo atapata ridhaa ya kuongoza tena Serikali, atahakikisha anamaliza changamoto ya maji na miundombinu ya barabara mkoani humo.
Dkt. Samia ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali yake imetekeleza miradi ya mbalimbali ya maji ikiwemo mradi uliojengwa Kata ya Butimba Wilaya ya Nyamagana kwa gharama ya shilingi bilioni 71.7, ambao ameeleza kuwa umewafikishia huduma ya maji safi na salama wakazi 450,000 wa Mkoa wa Mwanza.
Akinadi sera za CCM leo Oktoba 7, 2025, Dkt. Samia amesisitiza kuendelea kuboresha miundombinu ya maji mkoani Mwanza pamoja na kufanya upanuzi wa vyanzo mbalimbali vya maji kikiwemo cha Capri Point ili kuimarisha zaidi huduma za maji mkoani humo.
Katika sekta ya usafirishaji, ameeleza kuwa Serikali yake imekamilisha ujenzi wa barabara ya Buhongwa – Igoma yenye urefu wa kilomita 14 kwa gharama ya shilingi bilioni 22.7, ulioenda kwa pamoja na ujenzi wa madaraja ya Mkuyuni na Mabatini kwa shilingi bilioni 11.2, ambapo ameeleza kuwa ujenzi wa madaraja hayo unaendelea.
Dkt. Samia amesema akipewa ridhaa ya kuongoza tena atahakikisha anamaliza ujenzi wa barabara ya njia nne inayotoka Mwanza City Center – Buhongwa hadi Usagara kwa kiwango cha lami.
Pia ameahidi kuendeleza ujenzi na uboreshaji wa masoko mbalimbali ya mkoa huo likiwemo soko la Mchafu Kuoga, Soko la Samaki Mkuyuni, Soko la Mbao nyegezi, Soko la Mazao Igoma pamoja na mengine yaliyoko Mabatini, Buhongwa, Bugarika, Mbugani, Tambuka Reli na Butimba.