Katika mwendelezo wa kuhakikisha bunifu na biashara changa za vijana zinaendelezwa, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kwa kushirikiana na Sahara Ventures imekuja na programu ya kitaifa inayolenga kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini Tanzania.
Programu hiyo imepewa jina la ‘Tanzania Ventures Lab (TVL) itatekelezwa kupitia Kituo cha Teknolojia cha Dar Teknohama Business Incubators (DTBi) na Buni Innovation Hub, majukwaa ya kitaifa yaliyo chini ya Costech yanayohusika na kukuza ubunifu, teknolojia na ujasiriamali. katika hafla fupi ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Costech, Dk Amos Nungu amesema programu hiyo ya miaka minne inatarajiwa kunufaisha bunifu pamoja na biashara changa 1,000 za vijana katika sekta sita za kimkakati.
Nungu amesema kwa kila mwaka wanatarajia kuzishika mkono na kuziwezesha bunifu takribani 250 kutoka kwa vijana wanufaika.

Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike (kulia) na Mtendaji Mkuu kutoka Kituo cha Teknolojia cha Dar Teknohama Business Incubators (DTBi), Patience Karua (kushoto)
Hata hivyo lengo la programu hiyo ni kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini kwa kuunganisha wabunifu, watafiti, wawekezaji, sekta binafsi na taasisi za serikali katika mfumo mmoja wa kukuza na kuendeleza biashara changa.
