Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limetoa taarifa ya kumshikilia Wema Haibe (38), Dalali wa Mahakama, Kwa tuhuma za wizi wa kuaminiwa baada ya kuuza nyumba aliyokabidhiwa na Mahakama kisha kuiba fedha Milioni 22.
Taarifa ya Jeshi hilo imetolewa Novemba 14, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Safia Jongo, ikieleza kwamba Mtuhumiwa alielekezwa kuuza kwa mnada nyumba ya wanandoa Joseph Kalinda na Ndimira Kasisi iliyopo maeneo ya Fadhili Bucha, Kata ya Bahalahala, Wilaya ya Geita na kutakiwa kuweka fedha hizo katika akaunti ya Mahakama, ambalo ni takwa la kisheria.
”Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia Wema Haibe (38), Dalali wa Mahakama kwa Tuhuma za wizi wa kuaminiwa” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi hilo, April 4, 2025, mtuhumiwa aliuza nyumba hiyo kwa Tatizo Balanzila (56) kwa kiasi cha Milioni 22, ambapo kinyume na maelekezo ya Mahakama Mtuhumiwa huyo anadaiwa kuziweka fedha hizo katika akaunti yake binafsi badala ya akaunti ya Mahakama kama alivyoagizwa.
”Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina, na mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani mara baada ya taratibu zote za kisheria kukamilika ” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, taarifa ya Jeshi hilo imesema linaendelea kuchukuwa hatua kwa mujibu wa Sheria, huku likiwataka Wananchi pamoja na Madalali wanaotekeleza amri za Mahakama kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uaminifu na kufuata Sheria.