
Na William Mpanju- Biharamulo, Kagera
Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, SACP Advera Bulimba, ameongoza hafla ya kufunga Mafunzo ya 21 ya Jeshi la Akiba (Mgambo) kwa mwaka 2025 na kutoa onyo kali kwa viongozi wa vijiji na kata kutowadhalilisha askari wa jeshi la akiba.
SACP Bulimba aliwataka viongozi na wananchi kwa ujumla kuwaheshimu na kuwashirikisha askari hao akisisitiza kuwa ni sehemu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wanapaswa kutumika kikamilifu katika kudumisha amani na usalama wa jamii.
Aidha, ametoa onyo kali kwa viongozi watakaojaribu kugomesha mafunzo ya jeshi la akiba, akibainisha kuwa hatua hizo zitachukuliwa kama kukaidi agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameanzisha mafunzo hayo kwa lengo la kuandaa vijana kuwa wazalendo na walinzi wa nchi yao.
Akihutubia wahitimu, DC Bulimba amewapongeza kwa kuhitimu kwa nidhamu, umakini na utayari, akiwataka kwakawe mfano bora kwa jamii na kutumia mafunzo waliyopata kwa kuhudumia wananchi na kulinda usalama wa jamii.
Pia amewakemea wananchi wanaoeneza dhana potofu na maneno ya kuwadhalilisha askari wa mgambo, akisema vitendo hivyo vinadhoofisha ari ya uzalendo na juhudi za taifa kulinda raia na mali zao.
Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Biharamulo, Luteni Michael Chalamila, alisema kuwa mafunzo hayo yamehusisha kata tano za Runazi, Bisibo, Nyarubungo, Nyamahanga na Biharamulo Mjini
Jumla ya washiriki 136 wamehudhuria mafunzo, ambapo 122 wamehitimu rasmi na kula kiapo, wakiwemo wavulana 102 na wasichana 20. Washiriki 14 walishindwa kuhitimu kutokana na utovu wa nidhamu, utoro, na baadhi kuwa na utata wa uraia.
Mafunzo haya yanalenga kuandaa vijana kwa ajili ya kulinda amani, kudhibiti uhalifu na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.