
Na Samuel Samsoni- Kahama
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga Frank Nkinda ameagiza hatua za kisheria zichukuliwe kwa aliyekuwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Igomelo, Kata ya Malunga Manispaa ya kahama mkoani humo Laurent Benedicto endapo atabainika kuwa na hatia kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka kipindi alipokuwa kiongozi ikiwemo kuuza viwanja mara mbilimbili.
Kauli hiyo ameitoa Agosti 21, 2025 wakati akiendelea na ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi Wilayani humo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mwananchi Emanuel Maduhu ambaye anadai aliuziwa kiwanja na serikali ya mtaa huo kupitia kwa mjumbe maarufu “Afande Siro” (ambaye naye pia anatafutwa) ambaye majuma mawili baadaye kiwanja kile aliuziwa mtu mwingine.
Kwa upande wake aliyekuwa mwenyekiti huyo Laurent Benedicto amenukuliwa akisema kuwa kiwanja hicho kilikuwa na boma ndani yake na kilichouzwa ni kiwanja na siyo boma lililokuwemo na kudai kuwa kusema ameuziwa vyote ni kumuweka katika mgogoro.
Mkuu huyo wa Wilaya Nkinda ameliagiza Jeshi la Polisi Wilayani humo na kumkamata Mwenyekiti huyo mstaafu ili kuendelea na utaratibu wa kisheria dhidi yake sambamba na kutafutwa kwa “Afande Siro”.
Aidha Nkinda ametoa onyo kali kwa viongozi wa serikali watakao kuwa vyanzo vya migogoro vinavyo wachonganisha wananchi na Serikali yao ambapo amesema “nitalala nao mbele”.