
Baada ya Bahati kuachia video ya wimbo wake mpya Seti, ambayo inamuonesha akicheza na dansa wa kike aliyevaa mavazi ya kuacha wazi sehemu za mwili wake, mkewe Diana Marua ameandika taarifa rasmi akieleza kutoridhishwa na muelekeo mpya wa muziki wa msanii huyo.
Kupitia Instagram, Diana amechapisha taarifa isemayo, “My Statement on Bahati’s New Music Direction “Ninajitolea kikamilifu kwenye biashara zangu, ushirikiano wangu na chapa zinazoniamini.
Hiyo inamaanisha kubeba majukumu kwa njia inayodhihirisha ukuaji, uwajibikaji na maadili ninayosimamia. Kwa heshima ya familia yangu, washirika wangu na watu wanaoniangalia, sitahusiana na mwelekeo huu mpya wa Bahati katika muziki wake,” ameandika Diana.
Aidha amesisitiza kwamba anamheshimu mumewe kama msanii na safari yake ya kimuziki, lakini yeye binafsi hawezi kushiriki katika muelekeo huo na anaamini katika kusaidiana kama ‘couple’, lakini pia ana jukumu la kulinda taswira yake na nafasi anazojenga kibiashara na kijamii.
Hata hivyo, kutokana na historia ya wawili hao kutumia mitandao ya kijamii na matukio ya kiki kusukuma kazi zao, mashabiki wengi wamebaki na maswali, wakihisi huenda hatua hiyo pia ni sehemu ya mikakati yao ya kuvutia ‘attention’ kwenye muziki mpya wa Bahati.