
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema kuwa Tanzania inatarajia kuzalisha umeme unaotokana na nyuklia utakaojumuishwa katika Gridi ya Taifa ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya umeme yanayotokana na ongezeko la viwanda.
Dk. Biteko amesema hayo jana June 30, jijini Kigali nchini Rwanda wakati akihutubia Mkutano kuhusu masuala ya Nyuklia Afrika.
Amesema kuwa serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuandaa mikakati ya pamoja ya taasisi za serikali, ili kufikia azma ya kuzalisha umeme wa nyuklia kwa kuwa ni nishati yenye unafuu wa gharama kulinganisha na vyanzo vingine vya nishati, pia isiyochafuzi kwa mazingira.
Ametaja baadhi ya jitihada kuwa Juni 2025 Tanzania iliandaa warsha ili kutoa uelewa kwa wadau wa masuala ya nyuklia ikiwa ni pamoja na kuanzisha taasisi itakayoratibu na kusimamia shughuli za nyuklia.
Aidha Dk. Biteko amesisitiza kuwa Serikali itahakikisha inaendeleza mazingira mazuri kwa ajili ya uzalishaji wa nishati kwa kutumia nyuklia kwa kutunga sera thabiti na kuanzisha mifumo ya sheria na udhibiti kwa ajili ya usimamizi wa raslimali ya nyuklia na uzalishaji wa umeme unaotokana na nyuklia