
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania inalaani kuibuka upya kwa ukiukwaji wa sheria za kimataifa na kupelekea matumizi ya nguvu kama njia ya kutatua migogoro hali inayopelekea ukatili uliokithiri kwa binadamu hususani watoto, wanawake, wazee pamoja na wagonjwa katika maeneo ya migogoro.
Dkt. Mpango amesema hayo wakati akihutubia Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) kinachofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.
Amesema uwepo wa mitazamo ya kibeberu, ikiwa ni pamoja na ile ya kuichukulia Afrika kuwa sehemu ya uchukuaji rasilimali na uporaji wa ardhi, pamoja na uwepo wa makampuni ya kimataifa kuendelea kufanikiwa kutokana na unyonyaji wa mali asili za Afrika, huku wakisababisha au kuunga mkono migogoro inapaswa kumalizika sasa.
Makamu wa Rais amesema Tanzania inauchukulia msimamo wa upande mmoja na matumizi mabaya ya nguvu za kijeshi, pamoja na kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa na mataifa yenye nguvu duniani katika kukomesha umwagaji damu na vita vya hatari vinavyoendelea katika maeneo mengi duniani, kuwa ni jambo lisilokubalika.
Pia Makamu wa Rais amesema dunia inapaswa kuendelea kutafuta amani bila kuchoka kwani ndio sharti la maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha amepongeza juhudi za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa dunia, na mashirika ambayo yanashiriki kikamilifu katika upatanishi na utatuzi wa migogoro katika nchi na maeneo kama vile Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan, Urusi, Ukraine, na Mashariki ya Kati.
Amesema Tanzania kama mwanachama wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, pia nafasi iliyotumikia kama Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa Ulinzi na Usalama Jumuiya ya SADC ilichangia kikamilifu katika mipango ya amani na kuunga mkono hatua za kuzuia na kutatua migogoro.
Tanzania imetangaza kugombea kiti kisicho cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa muhula wa 2029-2030, ili kuthibitisha dhamira iliyonayo ya amani na usalama duniani.