
Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema ili kudhibiti janga la njaa na umasikini pamoja na kuharakisha maendeleo vijijini, ni vema mataifa kushirikiana kwa kuwa masuala hayo ni janga la linalovuka mipaka ya nchi.
Makamu wa Rais ametoa wito huo alipokuwa akihutubia wakati wa majadiliano kuhusu ‘Muungano wa Kimataifa dhidi ya njaa na sera za umma kwa usalama wa chakula’ kwenye mkutano wa pili wa Brazil na Afrika kuhusu Usalama wa Chakula, Mapambano dhidi ya Njaa na Maendeleo Vijijini uliofanyika Jijini Brasilia, Brazil.
Amesema madhara ya umasikini na njaa ni makubwa na yameathiri zaidi bara la Afrika licha ya uwepo wa rasilimali za kutosha.
Dkt. Mpango amempongeza Rais Luiz Inácio Lula da Silva wa Brazil kwa juhudi alizozianzisha kuunganisha mataifa na kuhamasisha ushirikiano huo kujidhatiti baina ya mataifa tajiri na yale yanayoendelea.
Makamu wa Rais amesema Brazil itakuwa mshirika mzuri kwa nchi za Afrika katika kilimo cha mazao na maendeleo vijijini kutokana na matumizi ya teknolojia nchini humo pamoja na hatua kubwa iliyofikia katika sekta mbalimbali.
Majadiliano kati ya Brazil na nchi za Afrika ni ya pili katika mzunguko wa majadiliano ya namna hiyo, ambapo majadiliano ya kwanza yalifanyika mwaka 2010 nchini Brazil, na yamekuwa yakiandaliwa na Serikali ya Brazil kupitia Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Ushirikiano wa Kiufundi la Brazil (ABC) pamoja na Shirika la Utafiti wa Kilimo la Brazil (EMBRAPA).