
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi, ameziagiza wizara zinazosimamia biashara Bara na Visiwani kuhakikisha wazalishaji viwandani wote nchini wanatumia nembo ya Tanzania katika bidhaa zao ili kutangaza zaidi bidhaa za Tanzania kimataifa.
Ametoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua rasmi Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya 49 ya Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba, sambamba na nembo ya biashara inayotambulisha bidhaa za Tanzania, yaani Made in Tanzania.
Dkt. Mwinyi amesema kila mzalishaji wa ndani lazima atumie nembo hiyo ili kuzitangaza bidhaa za Tanzania kimataifa na kuzifanya zitambulike pia.
Aidha, ameipongeza TanTrade kwa namna walivyokuwa wabunifu na kuyaongezea thamani maonesho hayo kila mwaka, na hata maonesho mengine yanayofanyika nje ya nchi, huku akitolea mfano Maonesho ya Japan ambapo Tanzania inaendelea kufanya vizuri na kutembelewa na wageni wengi zaidi.