Mwanamuziki nyota wa Uganda Eddy Kenzo amedai kuwa kampuni kubwa za muziki duniani zikiwemo Warner Music, Sony Music, Disney, na Universal Music Group zimewasiliana naye zikimtaka asaini mikataba minono.
Kenzo amesema Warner Music ilimpa ofa nono ya USD $1 milioni.
Hata hivyo, licha ya fedha hizo kumvutia, Kenzo alichagua njia ambayo wasanii wengi huiogopa kubaki msanii huru (independent).
Kenzo amesema uamuzi wake umetokana na kile ameona katika tasnia ya muziki duniani, akieleza kuwa label kubwa mara nyingi huwapa wasanii ahadi za kutamba kimataifa na kupata mafanikio ya kifedha, lakini nyuma ya pazia huwaweka katika masharti magumu ya ubunifu na kifedha.
Kenzo ambaye mwaka huu ametajwa kuwania tuzo za Grammy aliongeza kuwa hata baada ya mkataba kuisha rasmi, label bado huendelea kumdhibiti msanii hadi malengo ya kifedha yatimie.
Kenzo alimtolea mfano mkali wa Nigeria Tekno Miles, ambaye aliwahi kutawala muziki wa Afrika, lakini akawa kimya baada ya kusaini na label kubwa kama Universal.
Kenzo amesema Tekno ni mfano hai wa jinsi mikataba mikubwa inaweza kuua kasi ya msanii badala ya kuiongeza.