
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amesema Tanzania ni sehemu salama na yenye fursa nyingi kwa uwekezaji.
Ameyasema hayo wakati akifungua Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Marekani jijini New York, kando ya Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa sekta binafsi ni mshirika muhimu wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha Dkt. Mpango amesema serikali imeboresha sheria, miundombinu na mazingira ya biashara ili kuvutia wawekezaji zaidi.
Amesema Tanzania imekuwa na utulivu wa kisiasa kwa zaidi ya miaka 60, huku ikiboresha miundombinu na kupunguza urasimu, ikiwemo kupunguza muda wa usajili wa biashara kutoka siku 14 hadi saa 24.
Pia ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Marekani kuwekeza katika sekta za madini, nishati safi, kidijitali, kilimo, afya, miundombinu na utalii.
Ametaja uwepo wa madini muhimu kama graphite, nikeli na lithium, ambayo ni nyenzo muhimu kwa mapinduzi ya teknolojia na nishati safi. Aidha, amewakaribisha wawekezaji kushirikiana na Watanzania katika teknolojia za kilimo janja na usindikaji mazao.
Jukwaa hilo limehudhuriwa na wawekezaji kutoka pande zote mbili, ambapo Marekani imeipongeza Tanzania kwa sera thabiti na mazingira rafiki ya uwekezaji.