
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania Gilead Teri amesema hamasa ya wawekezaji kuwekeza nchini imeendelea kuwa kubwa hata katika kipindi ambacho nchi yetu ipo kwenye uchaguzi jambo linaloashiria imani kubwa ya wawekezaji hao kwa serikali.
Teri ameyasema hayo leo Oktoba 6, 2025 alipokuwa akizungumza na wanahabari kueleza hali ya Uwekezaji nchini katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026.
“pamoja na kwamba nchi yetu ipo kwenye uchaguzi hakuna punguzo la kasi ya uwekezaji na sisi kwenye uchumi tunaitafsiri kama imani ambayo wafanyabiashara na wawekezaji kote duniani wanayo juu ya Mheshimwa Rais pamoja na serikali kwamba hakutakuwa na changamoto zozote katika uchaguzi na baada ya uchaguzi” anesema Teri
Teri ameongeza kuwa imani hiyo ya wawekezaji inadhihirisha kuwa Tanzania ni sehemu salama kuendelea kufanya uwekezaji hata kama nchi ipo kwenye uchaguzi ni jambo la kipekee.
Ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo nchini ili kunufaika na fursa hizo badala ya wageni.