
Majaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC, wameanzisha uchunguzi dhidi ya Hungary kwa kushindwa kumkamata Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliyeitembelea nchi hiyo mapema mwezi huu.
Katika jalada lililowekwa wazi wiki hii, mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague-Uholanzi ilianzisha kesi za kutofuata sheria kwa Hungary baada ya kumkaribisha kwa heshima zote Netanyahu licha ya waranti wa kukamatwa kutokana na uhalifu dhidi ya ubinadamu unaohusishwa na vita vya Gaza.
Wakati wa ziara hiyo, Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orbán alitangaza kuwa nchi yake itajiondoa kwenye Mahakama hiyo akidai kuwa ICC si tena mahakama isiyo na upendeleo na inayotii sheria, bali imegeuka mahakama ya kisiasa.