
“Usichokifahamu ni kama usiku wa kiza”, “Fahari ya ng’ombe ni mkia, fahari ya mwanadamu ni akili.”
Kagera Tanzania – Kumasi Ghana-Usemi huu wa wahenga unafichua pazia la utajiri usiothaminika unaopatikana katika tamaduni zetu. Ingawa ulimwengu unazunguka kwenye mhimili wa sayansi na teknolojia, bado kuna vito vya zamani vinavyong’aa, na mojawapo ni majani ya magimbi.
Kwa mujibu wa tamaduni, hasa barani Afrika, mimea hii imekuwa ikihusishwa na matumizi mbalimbali. Sehemu kadhaa, kama desturi zinavyotofautiana, majani ya magimbi huishia kuwa malisho ya kuku, au hata hutumiwa kama kifungashio cha bidhaa sokoni. “Fahari ya ng’ombe ni mkia, fahari ya mwanadamu ni aklili,” usemi mwingine wa wahenga, unatuita kutumia akili zetu kutambua umuhimu wa kile tunachokipuuza.
Kutoka Kifungashio Hadi Mlo wa Kifalme
Swali la msingi ni hili: Je, majani ya magimbi/majimbi (Nduma) ni chakula kama ilivyo majani ya maboga, tembele, au kisamvu? Jibu linapatikana katika safari za mtembezi. Kwani wahenga walisema, “kutembe kwingi kuona mengi naye mtembea bure si sawa na mkaa bure.” Mwandishi wa makala haya alipata fursa ya kutembelea familia moja hapa nchini Ghana, kwenye jiji la Kumasi. Alichokikuta kilikuwa ni mlo safi wenye heshima kubwa, ambapo mboga kuu ya majani ilikuwa ni majani ya magimbi/ majimbi.
Familia hii ilikumbatia falsafa kwamba “Lishe ni dawa na dawa ni lishe,” wakitumia majani haya kutengeneza kitoweo kitamu na chenye virutubisho. Hii inakinzana na baadhi ya tamaduni za Afrika Mashariki, ambapo magimbi/majimbi yenyewe (kiazi) ndiyo huliwa, na majani kutupwa au kuwa malishio ya ndege mfano bata na kuku.
Licha ya kwamba majani haya yana tabia ya kuwasha pindi yanapoliwa, uuandaaji wake huvumbua hazinakubwa Iliyojificha iliyosheheni faida kadha wa kadha za Kiafya.
Ili kuondoa kiza cha kutokujua, watafiti wachache wameanza kuchimba utajiri wa virutubisho katika majani haya. Matokeo yanaonyesha kuwa majani ya magimbi yana hazina kubwa ya:
Vitamini A na C: Hizi ni nguzo za kinga ya mwili na hupigana na maradhi mbalimbali. Kama wahenga walivyosema, “Kinga ni bora kuliko tiba.” Pia, madini (mfano Chuma na Follati): Muhimu kwa uundwaji wa damu na kuzuia upungufu wa damu hupatikana na ulaji wa majani ya majimbi. Faida nyingine ni Fiber (Majaramba): Husaidia mfumo wa mmeng’enyo wa chakula kufanya kazi vizuri. Kwa maneno mengine, unapokula majani ya magimbi, unakumbatia falsafa ya “Kila mwamba ulioinama hufichua siri,” ukijifunza kuwa mema mengi hujificha katika vitu vinavyopuuzwa.
Je, utabadilisha mtazamo wako kuhusu majani ya magimbi sasa? Au utaendelea kuamini kwamba “Mchagua jembe si mkulima” kwa kuyapuuza? Katika tamaduni unamotokea, ni nini haswa matumizi ya majani ya majimbi? Tueleze maoni yako huku ukijua kwamba hakuna tamaduni iliyo bora kuliko nyingine. RK itakuwa inaendelea kutafuta wataalamu lishe kuweza kueleza kwa kitaalamu zadi, namna ya uuandaaji na ulaji wa majni ya magimbi/majimbi alimaarufu kama nduma.