
Huduma za uokoaji zinaendelea kuwaokoa takribani watu 21 waliofukiwa na kifusi katika Mgodi mdogo wa Madini ya dhahabu, unaomilikiwa na kikundi cha Wachapa kazi Kijiji cha Mwongozo wa Nyandolwa, uliopo mkoani Shinyanga.
Kwa mujibu wa Mkuu wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro amesema tukio hilo limetokea August 11, 2025 majira ya saa nne asubuhi wakati mafundi wakiufanyia ukarabati mgodi huo na kwamba mpaka jana watu watatu walikuwa wameokolewa na mwingine mmoja ameokolewa asubuhi ya August 13, 2025.
Mtatiro amesema kuwa wakati tukio hilo linatokea kulikuwa na watu 25 kutoka kwenye maduara matatu tofauti kwenye mgodi huo waliofukiwa wafukiwa na kifusi hicho.
Amesema kuwa katika duara namba 106 lilikuwa na watu 6, duara namba 103 kulikuwa na watu 11 na duara namba 20 watu wanane na zoezi la uokoaji linaendelea.
Naye Mkuu wa mkoa wa huo Mboni Mhita amefika eneo la tukio na kuwataka wananchi kuwa watulivu na kwamba wanachokifanya sasa wataalam wa kikosi cha zimamoto na uokoaji ni kutengeneza njia ambayo ni salama zaidi kuweza kuwafiki watu hao licha ya kuwepo Changamoto ya eneo hilo kuwa na mawe mengi toauti na maeneo ya uchimbaji ambayo ni teketeke.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa mkoa wa Shinyanga ametoa wito wa ukarabati wa mashimo ya machimbo ya madini kabla ya shughuli za uzalishaji kuanza.