
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amesema Kanisa Katoliki halina ugomvi na Serikali na kuwataka wanaohangaika kudhani kwamba kanisa lina malumbano na Serikali waachane na dhana hiyo.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema hayo wakati akihitimisha adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Mapadre wa jimbo hilo, iliyofanyika katika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, Msimbazi jijini Dar es Salaam.
“Kwa hiyo wale wanaohaingaika wakidhani kwamba Kanisa Katoliki linataka kushindana, kulumbana au kushikana mieleka na Serikali watambue kwamba sisi hatuna mpango huo. Kwa hiyo tamko hili langu liwasaidie muwe na uelewa sahihi na mfuate msimamo sahihi,” amesema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Aidha, Askofu Mkuu Ruwa’ichi amekanusha waraka uliosambazwa mitandaoni ukieleza kwamba Oktoba 29,2025 Jimbo Kuu la Dar es Salaam limeandaa Semina ya Walei itakatofanyika katika Parokia ya Kristo Mfalme, Tabata na kusisitiza kuwa ni taarifa za kughushi na hazitoki katika ofisi yake.
“Ninaomba kutamka pia jambo lifuatalo, wale mnaotumia vilonga longa, wale mnaopita pita kwenye mitandao, mtafahamu kwamba kuna jambo ambalo kwa siku hivi karibuni limekuwa likisambaa katika mitandao, ni tangazo lililotolewa kuhusu semina ya walei.
Naomba nitamke awali ya yote kwamba tangazo hilo halikutolewa na ofisi yangu,” amesema na kuongeza kuwa “Kwa hiyo siyo tangazo linalobeba sahihi yangu au lililotangazwa kupitia kwa chancellor au Katibu Mkuu, hilo liwafanye mtambue kwamba siyo tangazo rasmi.”
Amefafanua kuwa semina hiyo iliyoelezwa katika tangazo hilo feki kwa mujibu wa kalenda ya Jimbo, imepangwa kufanyika Novemba 29, 2025 na siyo Oktoba kama ilivyoelezwa katika tangazo hilo.
Hivi karibuni kumekuwa na waraka uliokuwa ukisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ukieleza kwamba waumini wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam watakuwa na semina itakayofanyika Oktoba 29, 2025, siku ambayo imepangwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya kupiga kura kumchangua Rais, wabunge na madiwani