
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, amesema kuwa Kanisa Katoliki linapaswa kuendelea kuwa nguzo ya matumaini kwa jamii, hasa kwa wanyonge wasio na sauti.
Padre Kitima ameyasema leo Juni 03, 2025 wakati akiongoza Misa ya Shukurani katika Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, lililopo makao makuu ya TEC, Kurasini jijini Dar es Salaam
Ibada hiyo imefanyika, kwa mara ya kwanza tangu aruhusiwe kutoka hospitali alikokuwa akipatiwa matibabu kwa takriban mwezi mmoja, kufuatia tukio la kushambuliwa na watu wasiojulikana ambayo imehudhuriwa na mapadri, watawa na wafanyakazi wa Sekretarieti ya TEC waliokusanyika kumshukuru Mungu kwa uponyaji wa Padri Kitima.
Akizungumza wakati wa mahubiri, Padri Kitima amesema, anamshukuru Mungu kwa uponyaji kwa sababu shambulio lake lilikuwa na lengo la kukatisha maisha yake.
Pia amewapongeza na kuwashukuru wote waliokuwa naye kwa sala, upendo na matashi mema wakati wote wa matibabu na kuwataka wafanyakazi wa Sekretarieti ya TEC kuyatazama yaliyotokea kwa jicho la kiimani na kuendelea kusimama imara licha ya changamoto.