Morocco imetangazwa kuwa bingwa wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kubatilisha matokeo ya kipigo chao kwenye fainali dhidi ya Senegal kufuatia tukio la utata la kutoka uwanjani.
Senegal iliifunga Morocco bao 1-0 kwenye fainali iliyochezvwa Januari 18, 2026, katika mechi iliyogubikwa na sintofahamu baada ya wachezaji wa Senegal kugoma kuendelea kucheza kufuatia waandaaji kupewa penalti dakika za majeruhi huku matokeo yakiwa bado 0-0.

Baada ya kusimama kwa takriban dakika 17, wachezaji wa Senegal walirejea uwanjani ambapo penalti ya Brahim Diaz iliokolewa, kabla ya Pape Gueye wa Senegal kufunga bao la ushindi katika muda wa nyongeza.
Hata hivyo, matokeo hayo sasa yamebatilishwa na chombo kinachosimamia soka barani Afrika. Katika taarifa yake, CAF imesema Senegal imechukuliwa kuwa imepoteza mechi ya fainali kwa kujitoa na kwamba matokeo ya mechi yameandikwa kuwa ushindi wa mabao 3-0 kwa Morocco.
Uamuzi huo umefuatia rufaa iliyowasilishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Morocco (FRMF), ambayo CAF imesema imekubalika kisheria na imeamuliwa kwa faida yao.

CAF imeongeza kuwa, Senegal ilikiuka Kifungu cha 82 cha kanuni za AFCON, jambo lililosababisha kutumika kwa Kifungu cha 84.
Kifungu cha 82 kinaeleza kuwa ikiwa timu itakataa kucheza au itaondoka uwanjani kabla ya muda wa kawaida kuisha bila ruhusa ya mwamuzi, itachukuliwa kama imepoteza na itaondolewa kwenye mashindano.
Kifungu cha 84 kinaongeza kuwa timu yoyote itakayokiuka Kifungu cha 82 itaondolewa kabisa kwenye mashindano na kupoteza mechi hiyo kwa mabao 3-0.
