Uongozi wa Soko Kuu la Kariakoo umesema takribani asilimia 70 ya wafanyabiashara waliopangiwa vizimba na maduka katika soko jipya tayari wameanza kufanya biashara zao.
Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, Ashraph Abdulkarim, amesema wafanyabiashara wote 1,520 waliokuwa wakifanya biashara katika soko la zamani lililoungua wamepatiwa nafasi katika soko jipya.
Soko hilo lilijengwa upya kwa gharama ya Sh bilioni 28 baada ya kuungua Julai 10, 2021 na kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Februari 8 mwaka huu.
Abdulkarim amesema asilimia 80 ya maeneo ya biashara katika soko hilo yametengwa kwa wafanyabiashara waliokuwa katika soko la zamani, huku asilimia 20 iliyobaki ikitangazwa ili kupata wapangaji wapya.
Aidha amesema kuwa kati ya wafanyabiashara 1,900 waliokuwa wakifanya biashara awali, wafanyabiashara 1,520 walirudi na kupewa nafasi katika soko jipya, huku nafasi zilizobaki zikitarajiwa kutolewa kupitia mnada.
Amesema utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais Samia wakati wa uzinduzi wa soko hilo umefikia zaidi ya asilimia 95 ambapo Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuanzishwa kwa kanzidata ya wafanyabiashara na matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato.
Pia ameeleza kuwa hatua zimechukuliwa kuzuia viongozi kuhodhi vizimba kwa kuwa nafasi zote zilitangazwa rasmi na kila mfanyabiashara alikuwa na fursa sawa ya kupata au kukosa.
