Kenya imepinga ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu tuhuma za ubakaji dhidi ya maafisa wake wanaohudumu nchini Haiti chini ya Ujumbe wa Kimataifa wa Usaidizi wa Usalama wa Kimataifa.
Katika barua iliyotumwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres tarehe 7 Aprili, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Kenya Musalia Mudavadi ameelezea wasiwasi wake kuhusu madai ya unyanyasaji wa kingono na dhuluma ambayo yaliripotiwa Agosti 2025.

Mudavadi amesema madai hayo yalichunguzwa mara moja kupitia Bodi ya Uchunguzi na kupatikana kuwa hayana uthibitisho.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni ameongeza kuwa wafanyakazi wa MSS walifuata kikamilifu mifumo yote ya uendeshaji na kwamba hakuna ripoti zilizobainisha utovu wa nidhamu.
Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutoka Februari na kuwekwa hadharani mwezi Aprili inaeleza maafisa chini ya ujumbe unaoongozwa na Kenya nchini Haiti walihusishwa katika visa vinne vya unyanyasaji wa kingono na unyanyasaji wa aina nyingine.
Ujumbe unaoongozwa na Kenya, uliotumwa Haiti mwaka 2024 kusaidia kukabiliana na ghasia za magenge, kufuatia idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, sasa nafasi yake imechukuliwa na Kikosi cha Kukakabiliana na Magenge.
