Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Methusela Ntonda, amesema kuwa kuongezeka kwa utambuzi wa lugha ya Kiswahili duniani ni miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana na wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Ntonda alisema kutambuliwa kwa Kiswahili kama moja ya lugha rasmi za UNESCO mwezi Novemba 2025 ni hatua muhimu katika kukuza hadhi ya lugha hiyo kimataifa pamoja na kuimarisha utamaduni wa Tanzania duniani.
Aidha, alitaja mafanikio mengine ya sekta ya utamaduni kuwa ni pamoja na kutambuliwa kwa muziki wa Singeli kama sehemu ya urithi wa utamaduni wa dunia, pamoja na kuendelea kwa kampeni za uhamasishaji kwa umma kuhusu historia ya harakati za ukombozi wa Afrika.
Ntonda alitoa kauli hiyo leo wakati akizindua Baraza la Wafanyakazi katika ukumbi wa wizara hiyo uliopo Mtumba jijini Dodoma. Katika hafla hiyo aliwataka wajumbe wapya waliochaguliwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, uadilifu na uwajibikaji, ili kuleta matokeo chanya kwa niaba ya wafanyakazi wa wizara hiyo.
Akizungumzia sekta ya michezo, Ntonda alieleza mafanikio kadhaa yaliyopatikana, ikiwemo Tanzania kupata haki ya kuwa mwenyeji wa michuano ya CHAN 2025, pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya mpira wa miguu na vituo vya mazoezi.
Aliongeza kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya maandalizi ya Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ambayo Tanzania itakuwa mwenyeji wake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Savera Kazaura, aliwapongeza viongozi na wajumbe waliochaguliwa katika baraza hilo, akitoa wito kwa menejimenti ya wizara pamoja na wakuu wa idara kushirikiana kikamilifu ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Mkutano huo pia ulihusisha uwasilishaji wa taarifa mbalimbali, zikiwemo mapitio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, mapendekezo ya mgawanyo wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027, pamoja na uchaguzi wa viongozi wa Baraza la Wafanyakazi.
