Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, ameagiza kuhamishwa kwa maofisa wa Polisi waliokuwa wakilinda watu mashuhuri na kupelekwa maeneo mengine ili kukabiliana na changamoto ya usalama nchini humo.
Hatua hiyo ya Rais Tinubu imekuja baada ya wanafunzi 50 kati ya zaidi ya 300 waliotekwa nyara kutoka katika Shule ya Katoliki nchini humo, kufanikiwa kutoroka kutoka mikononi mwa watekaji.
Tinubu amepokea taarifa hizo kwa furaha na kueleza kuwa anaendelea kufahamishwa kuhusu mwenendo wa hali ya usalama kote nchini.
Wakati huohuo, operesheni ya utafutaji na uokoaji inaendelea kwa ajili ya wanafunzi na walimu waliotekwa nyara na watu wenye silaha Ijumaa iliyopita. Shule katika eneo hilo zimeamriwa kufungwa kwa muda.
Kuongezeka kwa matukio ya utekaji nyara wa watu wengi kunakuja wakati ambapo utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani umewakosoa viongozi wa Nigeria kwa kile ilichodai kuwa kushindwa kuwalinda Wakristo dhidi ya mauaji yanayofanywa na wanamgambo wa Kiisilamu, madai ambayo serikali ya Nigeria imekanusha.