Jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, limetupilia mbali ombi la Mawakili wa Serikali la kuwasilisha ushahidi wa ziada kutoka kwa shahidi wa mpelelezi, ACP Amini Mahamba, katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Uamuzi huo umefuatia pingamizi lililowasilishwa na Lissu, akipinga hatua ya upande wa mashtaka kuomba kuongezwa kwa ushahidi huo wa ziada. Majaji wameridhia pingamizi hilo na kuamua kuwa ombi la Serikali halina msingi wa kisheria.
Kwa uamuzi huo, Lissu ameshinda pingamizi lake la msingi, akidai kuwa kuongezwa kwa ushahidi huo ni kinyume cha Kifungu cha 308 cha sheria, ambacho kinaelekeza utaratibu wa kuwasilisha ushahidi au kumwita shahidi mpya ambaye hakuwepo katika mwenendo wa awali wa Mahakama Kabidhi.
