Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Siasa Tanzania, Chadema, Tundu Lissu leo amefikisha siku 365 tangu akamatwe na kuwekwa gerezani kwa makosa ya uhaini na uchochezi.
Kutokana na hilo Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA wameendesha mjadala wa wazi kwa njia ya mtandao wakishinikiza Mwenyekiti wa chama hicho kuachiwa huru bila masharti wakidai kuwa kuendelea kushikiliwa kwake ni uminyaji wa haki za binadamu.

Mjadala huo umekutanisha viongozi wa CHADEMA akiwemo Makamu Mwenyekiti John Chacha Heche ambaye amesema, lengo la mjadala huo ni kushinikiza Lissu aachiwe huru.
Mjadala huo wa wazi, kadhalika ulijumuisha wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu na wanasiasa wa Kenya na Uganda, mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Ulaya (AFET) David McAllister, wanaharakati na wanahabari akiwemo Jenerali Ulimwengu, Maria Sarungi na marafiki wa chama hicho.
Tundu Lissu alikamatwa wilayani Mbinga, Ruvuma mnamo Aprili 9 mwaka 2025 akiwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika chini ya kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya chama hicho iliyopewa jina la tone tone.
CHADEMA, kimefanya kumbukizi hiyo kikieleza kuwa ni msingi wa kuimarisha demokrasia na kushikiniza kuachiliwa kwa kiongozi wao. Aidha Kesi ya Lissu ilianza kusikilizwa Feberuari 9 hadi Machi 6 mwaka 2026 katika hatua za ushahidi.
