Maafisa wa kijeshi nchini Guinea-Bissau jana Novemba 26 Jioni wametangaza kuipindua serikali ya Rais Umaro Sissoco Embaló na kumkamata wakati matokeo ya uchaguzi wa rais yalikuwa yakisubuiriwa kutanagzwa leo.
Maafisa hao wamejitokeza jioni kwenye televisheni ya taifa na kutangaza kuipindua serikali, kuchukua madaraka, kuifunga mipaka yote, kusitisha mchakato wa uchaguzi na kutangaza amri ya kutotoka nje.
Milio kadhaa ya risasi ilisikika katika mji mkuu wa Bissau karibu na ikulu ya rais ambaye amevieleza vyombo vya habari vya Ufaransa kuwa amepinduliwa yeye na maafisa wengine wa serikali na wakuu wa usalama wamekamatwa na kutiwa kizuizini.
Mpinzani mkuu wa rais Sissoko Embaló Bw Fernando Dias, na mgombea aliyeshindwa katika uchaguzi uliopita wa rais wa mwaka 2019 na Waziri Mkuu wa zamani Domingos Simoes Pereira nao pia wamewekwa kizuizini.
Mapinduzi hayo yamejiri siku tatu baada ya uchaguzi mkuu na siku moja tu kabla ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais uliokuwa na mchuano mkali kati ya Umaro Sissoko Embaló na mpinzani wake Fernando Dias ambao wote wanadai kushinda katika duru ya kwanza.
Mapinduzi ya Serikali katika mataifa ya Afrika limekuwa kizungumkuti na mapinduzi ya mwisho kabla ya Guienea Bissau yalifanyika Madagasika Octoba 12 mwaka huu ambapo Rais Rajoelina ameondolewa Madarakani.