Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohamed Omar amesema Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa mabadiliko ya kidijitali katika sekta ya elimu yanakuwa jumuishi, shirikishi na endelevu.
Dkt. Hussein ameyasema hayo Novemba 17, 2025 jijini Dodoma wakati akiongoza kikao cha majadiliano kuhusu muunganiko wa Mpango wa Msingitek na miradi mingine ya kitaifa inayotekelezwa katika elimu ya msingi, kikilenga kuongeza ufanisi na kuepuka urudufu wa juhudi.
Ameeleza kuwa Mpango wa Msingitek unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo, wakiwemo Imagine Worldwide, ambao wanatoa mchango wa kitaalamu na kifedha ikijumuisha vifaa vya TEHAMA, mafunzo kwa walimu pamoja na ushiriki katika ufuatiliaji wa matokeo ya utekelezaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Imagine Worldwide, Dkt. Jacqueline Mgumia, ambaye ni mtekelezaji wa mpango wa Msingitek, amewasilisha dira ya utekelezaji unaolenga kutumia TEHAMA kuimarisha ujifunzaji wa wanafunzi kwa zaidi ya shule elfu moja.
Amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mawasiliano ya karibu miongoni mwa wadau ili kuhakikisha utekelezaji unakwenda sambamba na malengo ya kitaifa na vipaumbele vya Serikali.