Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linachunguza chanzo cha moto mkubwa ulioteketeza mabweni mawili ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Sumve iliyopo Wilayani Kwimba mkoani hapo.
Tukio hilo limetokea Alhamisi Novemba 20, 2025 saa 7:13 mchana baada ya moto uliozuka wakati wanafunzi wakiendelea na masomo darasani.
Ambapo, uliteketeza mabweni ya Nkwame na Dk Magufuli ambayo yanatumiwa na wanafunzi wa shule hiyo kama makazi yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa katika taarifa yake kwa umma aliyoitoa leo Ijumaa Novemba 21, 2025 amesema hakuna mwanafunzi wala mtu mwingine aliyeripotiwa kujeruhiwa katika tukio hilo.
“Moto ulienea kwa kasi kutokana na uwepo wa vifaa vinavyowaka haraka kama magodoro, nguo, mablanketi na mali nyingine za wanafunzi waliokuwa wakitumia mabweni hayo,” amesema Mutafungwa.
Amesema Jeshi la Polisi, Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na wananchi walifika eneo la tukio kwa haraka na kufanikiwa kudhibiti moto kabla haujasababisha madhara makubwa zaidi.
“Baadhi ya mali ziliokolewa ikiwamo magodoro, tranka, mablanketi, ndoo za maji na viatu,” imesema taarifa hiyo.
Mutafungwa amesema uchunguzi wa chanzo cha tukio hilo unaendelea, huku ulinzi ukiimarishwa katika shule hiyo na shule nyingine jirani kwa kushirikiana na wananchi pamoja na uongozi wa shule.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali, limeanza uchunguzi kuhusu tukio hilo la moto. Tunatoa wito kwa wananchi watoe ushirikiano kwa jeshi letu ili kufanikisha uchunguzi,” amesema Mutafungwa.