Serikali imetenga zaidi ya Shilingi bilioni 45 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja matano ya kudumu mkoani Kagera ambayo awali yaliharibiwa na mvua za masika na kusababisha changamoto kubwa.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Joel Samwel Mwambungu ameambatana na watumishi wote kukagua miradi mitano ya ujenzi wa madaraja ya dharura inayotekelezwa katika Wilaya za Muleba na Bukoba, kufuatia athari za mvua za El Niño zilizonyesha mwaka 2024.
Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa daraja la Kanoni ambalo limekamilika kwa asilimia 100, Kyanyabasa asilimia 77, Kamishango asilimia 98, Kyetema asilimia 77, pamoja na daraja la Karebe lililofikia asilimia 73 ya utekelezaji.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mhandisi Mwambungu amesema ameridhishwa na kasi pamoja na ubora wa utekelezaji wa miradi hiyo, huku akiwaagiza wakandarasi kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilika ifikapo 20/2/2026 kama ilivyopangwa kwa kuzingatia makubaliano ya mikataba ya miradi hiyo.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi hiyo kwa lengo la kuwaondolea wananchi changamoto ya kukatika kwa mawasiliano ya barabara, hasa wakati wa msimu wa mvua kutoka na maji kuwa mengi.
Aidha, kukamilika kwa ujenzi wa madaraja hayo itachochea shughuli za kijamii na kiuchumi kuongezeka , kuboresha usafirishaji wa mazao na huduma mbalimbali, pamoja na kuharakisha maendeleo ya wananchi wa maeneo husika.
