
Na Shafiru Yusuph- Muleba, Kagera
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma limetembelea mradi wa shamba la Kahawa la Makongora lenye hekari 367 lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera na kujifunza namna ya upandaji wa miche.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma Bw. Fidel Chiiza amesema lengo la kutembelea shamba hilo ni kuona jinsi ya upandaji wa miche ya kahawa ambayo kanuni za upandaji zinaendana na zao la Parachichi.
Bw. Chiiza amesema kwa sasa Halmashauri ya wilaya ya Kakonko ina tarajia kulima kilimo cha Parachichi katika Kata ya Kasanda na kwanza ziara hiyo italeta tija katika kilimo kilimo hicho.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera Dkt. Abel Nyamahanga amesema tayari Wilaya hiyo imeweka kauli mbiu ya Nioneshe Unapolima ambapo kila mwananchi anatakiwa kuwa na shamba kwa ajili ya kulima mazao ya chakula na biashara, na zoezi hilo linawashirikisha maafisa ugani Vijiji na Kata.