Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu inayopatikana jijini Arusha, inatarajiwa kutoa hukumu ya kihistoria kesho, Ijumaa, Machi 6, 2026, katika kesi inayopinga uhalali wa mchakato wa uchaguzi mkuu wa Tanzania wa mwaka 2020.
Hukumu hiyo inasubiriwa kwa shauku kubwa kwani inahusisha ushahidi uliowasilishwa na viongozi wa upinzani, wagombea, na wapiga kura, wakidai kuwa Serikali ya Tanzania ilifanya vitendo vilivyokiuka haki za msingi za kura na kiraia wakati wa uchaguzi huo.
Kesi hii ilianzishwa mwezi Novemba 2020 na aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad ambae alifungua shauri hilo kupinga ukiukwaji mkubwa wa sheria za uchaguzi uliodaiwa kufanywa na chama tawala (CCM) na vyombo vya dola.
Baada ya kifo chake mwezi Februari 2021, Mahakama ilimridhia Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, kuendeleza shauri hilo kama mwombaji mkuu.
Wadai katika kesi hii, ambao wote ni raia wa Tanzania, ambao ni Ado Shaibu, wagombea wawili wa Ubunge na Baraza la Wawakilishi, pamoja na wapiga kura watatu walioandikishwa Malalamiko yao makuu yanajikita katika ukiukwaji wa haki za kisiasa na kiraia, madai ya matumizi ya nguvu na ukiukwaji wa misingi ya kidemokrasia na uhitaji wa kufanya mageuzi ya Katiba na sheria za uchaguzi nchini Tanzania.
Kwenye kesi hii, Mahakama ya Afrika inaombwa kutamka kuwa Uchaguzi Mkuu 2020 haukuwa halali kwa sababu ya kukiuka misingi ya kidemokrasia na haki za binadamu ikiwemo kuenguliwa kwa wagombea, kura feki, Tume ya Uchaguzi kukosa uhuru, mauaji ya raia, vyombo vya habari kukosa uhuru na vyama vya siasa kukosa usawa kwenye mfumo mzima wa uchaguzi.
Taarifa iliyotolewa na wanasheria wa wadai, akiwemo Fulgence Massawe (Tanzania), Chidi Odinkalu (Nigeria), na Ibrahima Kane (Senegal), inaeleza kuwa serikali ilichelewa kutoa utetezi wake na hata ilipofanya hivyo, ilikanusha madai hayo bila kuleta ushahidi wa kutosha.
Mwaka 2025, Mahakama iliruhusu vituo vya haki za binadamu vya kimataifa, ikiwemo Robert F. Kennedy Human Rights Centre, kutoa maoni yao kama “marafiki wa mahakama” (amici curiae) kutokana na uzito wa kesi hiyo.1h
